Saturday, November 5, 2011

Mikoa tusipoamka

Wajinga watatawala, mikoa tusipoamka,
Naitoa halahala, uchaguzi tunataka,
Ila pasiwe na hila, kiongozi kumuweka,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.




Ukiritimba watula, vigumu kuneemeka,
Uchama sasa ni hila, mikoa inavunika,
Na wajuu watawala, kile kisichostahika,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Shamba la bibi walola, viongozi wastahika,
Kila mmoja apula, kile anachokitaka,
Si mashamba si mihela, wazidi kutakasika,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Usimwamshe alolala, hilo wanalitamka,
Hawana kwako jamala, ila wao kulimbika,
Na hili kila pahala, hija sasa yafanzika,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Madaraka kijumla, lazima kujayashika,
Mikoa kujitawala, kiuchumi kwa hakika,
Rasilimali ni ghala, ziache kuja ibika,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Na huu si ukabila, kiongozi twamtaka,
Mkoa mwenye jamala, waziri mkuu kumweka,
Na mawaziri salala, wizarazo kuzishika,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Na hili sio suala, wakubwa rai kutaka,
Ni ukoloni wa msala, kuacha hawatayataka,
Wazidi kuwa madhila wadhani wanajengeka,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Watu acheni kulala, mikoa kutawalika,
Ubwege nao ufala, bado hamjauchoka,
Mikoa sio jalala, wabovu kujawaweka,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Tusiendelee kulala, mikoa ije jengeka,
Ujerumani kulola, haya yanavyofanyika,
Ni raha yangu Makilla, mikoa kuongozeka,
Mikoa tusipoamka, kuzidi kudidimia.

Udaktari si hoja

Kuna digrii za bandia, nyingine za kupewa,
Dukani huko India, si vigumu kununua,
Kisomo lebo haijawa,bali uwezo nao kuwa,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?



Wengi tunaowajua, udakta wajivunia,
Ndani ukiangalia, hawana wanalojua,
Kitu wangelitambua, masikini tusingekuwa,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Ni sponchi zilojaa, maji huya kumwaia,
Pulizo zilopepewa, upepo ndani kujaa,
Abyadhi kifungua, akili zimetopea,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Udokta bwana kujua, kila unachoangalia,
Na unayojisemea, kuhakiki unajua,
Na kila unachosikia, tathmini kukifanzia,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Hesabu huzitambua, japo hutozielewa,
Kujumlisha sanaa, na kuzidisha hatua,
Ni mtu wa kutambua, mfuko sio gunia,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Si wa kuwaitikia, wachimvi wanaolia,
Wanasiasa kugwaya, kufanza wanayoamua,
Japo ujinga wajua, bado unawatumikia,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Sio kashfa nazua, watu budi kujijua,
Nafasi kutochukua, mahala pasipowafaa,
Na ushaur kujitia, hali huna unalojua,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Huruma ninawaonea, dokta jina kupewa,
Wengi wachangamkia, hata tiba asilia,
Marais waingia, ni nyingi wajizolea,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Mawaziri nao pia, sasa wanajipatia,
Wengine wazinunua, nafasi kujiongezea,
Mbumbumbu walokuwa, sasa ni maprofesaa,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Ila anzali ajua, hujui hujayajua,
Na kilemba si kofia, na wigi sio upaa,
Kibla wanaojua, uongo hawatazua,
Udaktari si hoja, hoja umesoma wapi?

Vita viogopeni

Chanzo wasioamua, yapaswayo amuliwa,
Kwa wakati unaofaa, na haki kutengenea,
Siasa wanaotumia, visingizio kadhaa,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!


Waoga wa kuamua, shujaa wa kuongea,
Ujanja wanaotumia, mahala pasipofaa,
Na za mkato njia, watakaozitumia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Kadiri wasiojua, yatakiwa kugawiwa,
Ukiritimba kuzua, fikra unapoua,
Na mabavu kutumia, dhidi ya wao raia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Haambiliki balaa, hakuna wanalosikia,
Kaburi hujichimbia, huku wanajionea,
Na hutaka kuingia, na wale wanowafatia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Uwezo wasiokuwa, ila wingi wa tamaa,
Ukubwa wanaolilia, hata watu kuwaua,
Nafsi wasiojua, tayari kuangamia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Uchama wanaotumia, uhalali kujitia,
Wananchi kuwagawa, majinuni wasojua,
Na kisha kuwatumia, malengo yao kufikia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Ni watu walolaniwa, toka walipozaliwa,
Na Mola huwasaidia, motoni kuja ingia,
Na laiti walingejua,ukubwa wangeukataa,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Mamlaka wasoachia,pale wanapotakiwa,
Wakatafuta wabaya,kumbe wao ndo wabaya,
Bahaluli kutumia, mauti kuyaandaa,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Katiba wakiwambiwa, si wao kuiandaa,
Ulaghai wajitia, na kughushi washtakiwa,
Wawaacha wanasheria,wajifanya wanajua,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Ufisadi waulea, na mafisadi radhia,
Kwa mali wakiwafaa, chamani na nyumbani pia,
Na aibu wala haya, vigumu kujionea,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Ni watu wasosikia, sikio linalojifia,
Ushauri huambaa, mradi wakajifanyia,
Kilio kinachofatia, hakitawasumbua,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Ni muda kujiandaa, vijana wa Tanzania,
Nchi wanaochezea, lazima kuwafichua,
Kizazi kinachofatia, amani kikailea,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!

Thursday, October 20, 2011

Uhuru wa kiuchumi

Uchumi kuwa huria, twataka viranja wapya,
Fani wanaozingatia, na ustadi kujaliwa,
Wajifanyao wajua, hatutaki wasikia,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Nchi hii ni dunia, mipaka imesambaa,
Tunatakiwa mikoa, yote kujitegemea,
Huru ikaachiwa, uchumi kuunyanyua,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Asiwe wa kuteua, mkuu wetu wa mkoa,
Twataka kumchagua, kiongozi anayefaa,
Uchumi kuuinua, mkoa wetu ukapaa,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Awajibike jamaa, kwa wakazi wa mkoa,
Kama inavyoendelea, Ujerumani Ulaya,
Nchi imejigawa, huru mikoa ikawa,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Uwekezaji wakua, viwanda vyashindaniwa,
Uzalishaji wakua, na masoko yazagaa,
Hadi sasa wasaidia, homa waliozidiwa,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Magari washadidia, BMW mwazijua,
Mercedes Benz radhia, ndiko zinakotokea,
HIi mali ya mkoa, kwa nchi inachangia,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Kilimo wamekomaa, walima kiteknolojia,
KIla mkoa wazaa, cha kula na kujiuzia,
Mayuro wajivunia, na nchi inaendelea,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Biashara waingia, kimataifa wapaa,
China wanakouzia, vyombo vyaaminiwa,
Mjerumani kifaa, nani asiyemjua,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Ni mikoa kutumia, soko, viwanda kua,
Raia kugombania, wao vya kwao bora kua,
Ni heshima na ushujaa, zikiwa bora bidhaa,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Elimu wanaojua, watoto kutufundushia,
Mitaala kuchagua, nchi inayoiifaa,
Na masomo kupungua, si ya kikapu kujaa,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Huduma wlaiobobea, wafaa wao kutoa,
Pasiwe wa kulegea, kazi akakabidhiwa,
Nchi kuendelea, imara tunatakiwa,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Wazee watasogea, pembeni wakasinzia,
KIla wakishtuliwa, mambo wataangalia,
Nchi itasisimua, na wengine kuvutia,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Vijana kuangalia, wapi tuanelekea,
Nasi bila kubagua, nafasi kuwamwagia,
Na wale wanaojua, kutufikisha hatua,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Hakuna kupendelea, hata kwa tuliowazaa,
Kama wasipojua, vingine kuwasaidia,
Ila kama wanajua, wastahili kwendelea,
Uhuru wa kiuchumi, wataka vinara wapya!

Mapinduzi ya uchumi

Yote tisa sasa kumi, uchumi kuzungumzia,
Sio wewe sio mimi,hapa ndipo pakuanzia,
Nchi bila ya uchumi, siasa hazitafaa,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Mapinduzi ya uchumi, budi kuzungumzia,
Ni vipi tunajihami, utandawazi waingia,
Kuendelea si ngumi, ila uchumi kuzaa,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Kuizindua jamii, majukumu kuyajua,
Miundombinu na lami, barabara kupaua,
Tufanane na Miami, Marekani ilivyokua,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Mbona watu hatutumi, meli kujitengezea,
Treni nazo uchumi, twazitaka kunyanyua,
Na kwanini hatusemi, bandari kujijengea,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Iwe ni wewe na mimi, akili tunatumia,
Ufundi wetu rasmi, kazini ukaingia,
Kusaidiwa uvumi, Magharibi kwasinyaa,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Elimu yetu uchumi, yastahili sasa kua,
Matatizo kujihami, na fursa kuzitumia,
Ni wewe na mimi, twapaswa vitu kuvumbua,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Kwanini hatuwatumi, wana Uchina kujua,
Na njia hatuzifumi, kujifunza Malaysia,
Maslahi si salami, waijuayo Ulaya,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Kwanini hatujipimi, tuone tunapopwaya,
Nchi yataka ulimi, mapya unayozua,
Kisiasa kujihami, watu haijawasaidia,
Tuzungumzie pia, mapinduzi ya uchumi.

Ndoa na chama kimoja

KAMA mnavyotambua, upacha yetu tabia,
Mme na mke twajua, ni wawii kijinsia,
Na kushoto na kulia, ni pande mbili za njia,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Wabunge wanapojaa, bungeni kwenda kukaa,
Wote wa chama ikawa, basi jua hapo jaa,
Rahisi kurubuniwa, patupu ukaambulia,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

'Ndio' wataitikia, hata kama ni kukuua,
Ili mradi wapewa, posho zenye manufaa,
Haliyo hawatoijua, wala kuizingatia,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Vijijini mwaumia, chama mosi kuwaoa,
Vichwa vimewajaa, wenyeviti wasojua,
Kijiji kinadumaa, ni vigumu kuendelea,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Wanasiasa balaa, sikuzote huwahadaa,
Watoto huwadhania, hamtawashtukia,
Pipi mtazingojea, mwaishia kuzisikia,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Vyema ndoa kukataa, waume wawili wakawa,
Mkeo kimoja ikiwa, wewe cha pili kuingia,
Yanga na Simba kuwa, wallahi mtaendelea,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Kama nyote Yanga mwawa, nyumba itasinzia,
Au simba tu mkawa, huzubaa familia,
Msisimko hujaa, vyama vingi kuingia,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Chagua kuendelea, ukiritmba kataa,
Chama kimoja balaa, hakiwezi kukutetea,
Wao wenyewe hung'aa,wewe ukawa wafubaa,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Ushindani maridhia, ndivyo unavyotakiwa,
Pande mbili kuvutia, kule mtu alikokaa,
Na nchi inaposogea, hatuwapi wasiofaa,
Ndoa na chama kimoja, hukufikisha pabaya.

Ukiritimba

Udikteta ndoto mbaya, mjinga akija kuwa,
Akiongoza huumia,wajinga na wanaojua,
Ni watu wa kupepewa, na moto kukokewa,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Na huyu mtu akiwa, mwenyewe tu huamua,
Zimbabwe angalia, sasa kinachotokea,
Na Malawi kaingia, mtu tusiyemdhania,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Gaddafy haukujua, yaliyomfika Libya?
Mubarak anajuria, Misri aliyoyazua,
Na Kenya hukuijua, Moi alipsimamia?
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Museveni naye pia, haya hatukumdhania,
Uganda kaikomboa, na sasa anaibomoa,
UKubwa una hatia, kwa watu wasiosikia,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Muumba namshangaa, watu hawa kuvumilia,
Sijui anadhania, watakaa kujutia,
Akawapa msamaha, mauti hajawajia,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Hujifanya wanajua, hata wasiyoyajua,
Wengine huwadhania, mabaya kuwafanzia,
Kwao si kazi kuua, ukubwa kuutetea,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Shirika nalo balaa, dikteta huliua,
Ukititimba huzaa, maradhi yasiyotibiwa,
Hadi huja kusinyaa, lenyewe likajifia,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

TTCL angalia, ugonjwa hatujajua,
Ukimwi utadhania, wala hautaelewa,
Mbona wengine wang'aa, lenyewe lazidi fubaa?
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

TANESCO ni baa, giza na bei kupaa,
Hakuna asiyejutia, 'ovataimu' kuliua,
Wingi wa watu kujaa, na kazi zinazubaa,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

TRC ng'amua, na TAZARA inayosinyaa,
Ukiritimba waviua, ushindani unapwaya,
Mameneja wenye njaa, ni shamba la kujivunia,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Ukiritimba tabia, wananchi isyofaa,
Na hii ya chama ikiwa, wanachama huenguliwa,
Mamluki wakajaa, mifuko yao kujaa,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Na ujinga nahofia, hili unalisaidia,
Wafuasi wakijua, uongozi hupindua,
Udhaifu kukataa, na wengine kuchagua,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Chama kibaka kikiwa, nchi kuisanzulia,
Wananchi huwa wakiwa, wasijue pakukimbilia,
Nusura haitatokea, bila sauti kutoa,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Ni sauti ya kukataa, kwa hapo tulipofikia,
Mapinduzi kuyazua, watu wapya kwingia,
Afueni kuitwaa, nchi ipate endelea,
Ukiritimba mbaya, huongozwa na wajinga!

Tuesday, October 18, 2011

Binadamu haridhiki

Haridhiki mwanadamu, maisha yake fataki,
Huyatamani matamu, japo kazi haitaki,
Hutaka kutakadamu, kuondoka haondoki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?


Hatosheki mwanadamu, kwa mamia na malaki,
Mtu asiyeisha hamu,kulimbikiza hachoki,
Ingawa linamgharimu,kwake halieleweki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Mwenyewe hujidhulumu, kwa zake tambo na ashiki,
Maisha huyahujumu, akidhani astahiki,
Cha halali na haramu, kwake havifahamiki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Mkweli humlaumu, akampenda mnafiki,
Udugu kwake haudumu, akapenda marafiki,
Wasafi huwatuhumu,akaamini mamluki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Mke aliye adimu, humfanzia mikiki,
Akamfata mndimu, mzinzi mwenye hilaki,
Huikataa salamu, matusi akaafiki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Wazazi hawarehemu, hutaka kutamalaki,
Kwayo anayojihimu, yote yanamdhihaki,
Kama analo jukumu, nafsi haishibiki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Muumba akimkarimu, vijisenti kwa malaki,
Hakai kujiheshimu, dharau atahakiki,
Shukrani huwa adimu, hata kwa wake Maliki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Magari atadhulumu, mengi akayamiliki,
Hata kuitoa dumu, ya kafara hudiriki,
Huidharau hukumu, akayajali lukuki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Majumba atadhulumu, kila pande amiliki,
Mengine akakasimu, kwa changu na mashabiki,
Akamhini karimu, himidi na tabaraki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Nahofu yako hukumu, ewe Mujibu na Baki,
Nafsi nisidhulumu, nitosheke tu kwa hiki,
Kwa laili na kiamu, radhi yako na riziki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Menejimenti rahisi

WAGUMU ni binadamu, uongozi ni rahisi,
Na wakiwa na elimu, wepesi kwenye maasi,
Wale wasiofahamu, nao ni kama farasi,
Menejimenti rahisi, wagumu binadamu.

Kulea utaalamu, ni maongozi halisi,
Mwenyewe kujifahamu, hii ni kubwa sayansi,
Atajua majukumu, kwa wenzake kina nasi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Watu wakikutuhumu, kuwaongoza yabisi,
Wakikuona dhalimu, amri zako nakisi,
Na kama sio mwalimu, wanafunzi hukuasi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Silaha sio kalamu, ila kujaza nafasi,
Kwao kilicho muhimu, taliki ubinafsi,
Ukiwa mtu rahimu, hukwepuka nuksi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Kazi hii si kukaimu, yataka kutanafasi,
Kuyabeba majukumu, mbele yake ikhlasi,
Kunusuru wanadamu, budi kutokwa kamasi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Uongozi uimamu, haukubali maasi,
Kujua hili muhimu,kikamilifu si kipisi,
Kulimbikiza dawamu,ni laana na mkosi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Mipango budi idumu, wajibu wataka kasi,
Uratibu ni adhimu, nao hupima kiasi,
Uongozi ni jukumu, kwa njia kuziakisi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Daawa mustakimu, na isiyo na najisi,
Nasi haitugharimu, wala haina uyabisi,
Humfaa mhashamu, baraka kuwa fususi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Maamuzi ni muhimu, yakisukwa kiususi,
Yakalenga kinajimu,vitendo vyenye hamasi,
Kustawi wanadamu,bila mola kumuasi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Udhibiti si haramu, watu kukosa wepesi,
Twataka kutakadamu, na si nyuma kudurusi,
Wawekezaji adimu, wenye kuvaa libasi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Tumtangulize rahimu, ni wetu Afu Qudusi,
Katuumba binadamu, bali sisi twamuasi,
Ukhalifa tunakimu, watokeze wafuasi,
Menejimenti rahisi, wagumu ni binadamu!

Wajibu kutumikia

Wengine kutumikia, binadamu ameumbwa,
Hili ni kama sheria, haustahili kuombwa,
Kutuma na kutumiwa,kila mwomba huombwa,
Binadamu ameumbwa,wengine kutumikia.

Hautoifurahia, dunia usiyoombwa,
Pengine utashangaa, kitu gani umekumbwa,
Au utajidhania, ilviyo haukuuumbwa,
Binadamu ameumbwa,wengine kutumikia.

Porini ukibakia, na tufani umesombwa,
Wanyama hukwangalia, kama vile hujaumbwa,
Hawatakusogelea, bila ibra kuwambwa,
Binadamu ameumbwa,wengine kutumikia.

Au jangwani kwingia, na mchanga umesombwa,
Peke kiumbe ukawa, kwa hari utalambwa,
Upweke hukuzidia, ukajutia kuumbwa,
Binadamu ameumbwa,wengine kutumikia.

Jela walioingia, kwa kosa moja kubambwa,
Kuta zikawazuia, kujipamba na kupambwa,
Huwehuka wakalia, wafungwa wanavyochambwa,
Binadamu ameumbwa,wengine kutumikia.

Ndani ukijifungia, hata vipi kumerembwa,
Utumwa utajisikia, hadimu haujasombwa,
Uhuru ukalilia, nje uende kuwambwa,
Binadamu ameumbwa,wengine kutumikia.

Raha ni kutumikia, na sio bure kubebwa,
Fani hiyo yawafaa, wanaopenda kulambwa,
Yule anayejisikia, katu hawezi kufumbwa,
Binadamu ameumbwa,wengine kutumikia.

Sioni timu kujiunga

Klabu hakuna nchini, kilichopo ni utani,
Nijiunge timu gani, ushindi inayothamini,
Sio wa hapa nchini, bali kote duniani,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Haijastawi fani, hakika hapa nchini,
Mechi zetu zote duni, ya kuangalia sioni,
NInashindwa kiwanjani, kwenda kukaa juani,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Ukianzia golini, golikipa siwaoni,
Hawatoi tumaini, wakienda ugenini,
Njaa imewazaini, kukimbilia golini,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Mabeki kama katuni, sijui alowasaini,
Mpira waenda golini, wao hawalibaini,
Kufungwa kwao amini, hawawi masikitikoni,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Mawinga siwaoni, wajuao kimiani,
Wala hawana kanuni, na mfumo siubaini,
Wanitia mashakani, kufungwa hata nyumbani,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Mafowadi masikini, hawapo hapa nchini,
Wanatoka ugenini, hili jamani kwanini?
Nakiona kisirani, na balaa baluwani,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Makocha twawathamini, watokao ughaibuni,
Kazi yao siuoni, ila ujira makini,
Shahata kumbaini, bado hili ndotoni,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Tumgeukie Manani, michezoni tushaini,
Dua haiyamkini, ziilete afueni,
Tujulikane barani, kama sio duniani,
Sijiungi na klabu, isoshinda kimataifa.

Monday, October 10, 2011

Silipi wala sisepi

Sikuomba, umenipa, silipi wala sisepi!
Hili huwezi kukwepa, ni jembamba kama papi,
Usiulete mshipa,hujui tuko wangapi?
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Wengi walienda kapa, uliza ni mara ngapi?
Na kwenyewe hapa hapa, na wala hatuongopi,
Huwezi hesabu chupa, ukajalipwa kwa chupi,
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Je, unaye golikipa, na wafungaji wangapi,
Ushindi huwezi kopa, ukope benki ipi?
Utoacho umetupa, silipi wala sisepi,
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Nyenzo yako bado bapa, ukaionolee wapi?
Kenya shilingi ni chapa, kwetu madafu na pipi,
Fisi ukimshinda mfupa, watakaoula wa wapi?
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Moshi wavaa malapa, huku Buguruni vipi?
Mtoto sasa ni pampa, zimeshafubaa nepi,
Ninunualo hulipa, la kupewa sililipi,
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Sijahusudu Urapa, ya kwetu asili iwapi?
Ya wengine ukikopa, ribaye maisha mafupi,

Silipi wala sisepi

Sikuomba, umenipa, silipi wala sisepi!
Hili huwezi kukwepa, ni jembamba kama papi,
Usiulete mshipa,hujui tuko wangapi?
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Wengi walienda kapa, uliza ni mara ngapi?
Na kwenyewe hapa hapa, na wala hatuongopi,
Huwezi hesabu chupa, ukajalipwa kwa chupi,
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Je, unaye golikipa, na wafungaji wangapi,
Ushindi huwezi kopa, ukope benki ipi?
Utoacho umetupa, silipi wala sisepi,
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Nyenzo yako bado bapa, ukaionolee wapi?
Kenya shilingi ni chapa, kwetu madafu na pipi,
Fisi ukimshinda mfupa, watakaoula wa wapi?
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Moshi wavaa malapa, huku Buguruni vipi?
Mtoto sasa ni pampa, zimeshafubaa nepi,
Ninunualo hulipa, la kupewa sililipi,
Silipi wala sisepi, umenipa sikuomba!

Sijahusudu Urapa, ya kwetu asili iwapi?
Ya wengine ukikopa, ribaye maisha mafupi,

Ulisikiza umbeya

Ulisikiza umbeya, kisha ukauamini,
Ukweli hukuchungua, uamuzi kusaini,
Laiti ungelijua, ungefanya tathmini,
Ulisikiza umbeya, wito wako nakataa!

Wito wako nakataa, kwa sasa sikuthamini,
Cheo nimeshakuvua, ni kuruta wa kambini,
Abautani rejea, hutonikuta uani,
Ulisikiza umbeya, wito wako nakataa!

Nyikani hujatembea, utajua ya jangwani?
Ukweli hukuzoea, hakika utabaini?
Haki unaichezea, pepo ipi utawini?
Ulisikiza umbeya, wito wako nakataa!

Maiti nawatambua, wote waso nithamini,
Hata hai wangekuwa, kwangu hawana thamani,
Maisha hujiendea, Hai nikimtumaini,
Ulisikiza umbeya, wito wako nakataa!

Yakini sikuzaliwa, kuwa mchache wa imani,
Ila kumtumikia mtu hilo siamini,
Ni Muumba ya Alaa, mtumwa namuamini,
Ulisikiza umbeya, wito wako nakataa!

Ndiye wakunichagua, kwa anayoyabaini,
Mikono huitumia, kufanya yake yamini,
Na akili huteua, akanipa umakini,
Ulisikiza umbeya, wito wako nakataa!

Moyo huutangulia, pasiwe na uzaini,
Nalo analoamua, kumtii nathamini,
Kiumbe njia najua, sifuati ya shetani,
Ulisikiza umbeya, wito wako nakataa!

Kwa shani wanaozuka

Ni asili na hulka, mwanadamu kumfika,
Kila anayeinuka, hutamani kusifika,
Na jinale kutajika, hata lisipohusika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Hawaachi kuzuzuka, kwa shani wanaozuka,
Iwe ni kwa kuandika, au nyimbo kuimbika,
Wote wanahadaika, wakidhani watukuka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Wale wachezao soka, asu sinema kuchezeka,
Haya pia huwafika, yakawa makubwa mashaka,
Huvianzisha vibweka, mijini wakatajika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Kila kizuri hutaka, na vyeo kujipachika,
Hata shule wasofika, uprofesa hutaka,
Wale wasioumbika, umalaika hutaka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Magari wakiyashika, hudharau zote rika,
Na ajali za kupika, haziachi kuwacheka,
Marehemu hugeuka, mkosaji kwa alofikwa,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Elimu yahitajika, vijana wetu kupika,
Waache kuja zuzuka, wawe wanaostahika,
Bilioni wakishika, wajue zinakohitajika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Msichana kusifika, si waume kukutaka,
Na mme kujatajika, si makoo yote kupoka,
Uungwana si dhihaka,na ukubwa ni mashaka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Maisha yana haraka, yanini kuhangaika,
Mbali hautofika, na dunia hukucheka,
Nayo japo waitaka, yenyewe haitakutaka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Zuzuka kwake Rabuka, nawe utatajirika,
Wala hutohangaika, na chochote kukitaka,
Utakuwa watosheka, japo umefilisika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Tukidhi mengi hakika, ila si ya kusifika,
Tunatambua Rabuka, ni wewe tu msifika,
Haya tunayoandika, ni kwako yanakotoka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Kulikoni ya ukwasi

Kulikoni wasiwasi, niepushe na dhuluma,
Siuhitaji ukwasi, nijalie wana wema,
Niepushe na kamasi, kuhesabu ndarahima,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Niepushe na yabisi, nipe moyo wa huruma,
Nifanze niwe msusi, wa kila jambo adhama,
Na nifanye mrahisi, kwa andiko na kalima,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Nusuru ngozi nyeusi, kwa wana walio wema,
Wape wakwangu sudusi, Alwaqiah kuzama,
Wawe watu wa kiasi, na wanyonge kutazama,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Wawe ni watu halisi, kuwajali mayatima,
Utu kwao udurusi, kwa zama mpaka zama,
Hadi siku abunusi, jichole kuwatazama,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Masikini wasiasi, kwao ni baba na mama,
Tulitoka huko nasi, mgongo kuwapa si vyema,
Wawashike kadamnasi, hata wasio heshima,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Wakinge na maasi, katika za kwetu zama,
Kwa tabia na libasi, wape kila kilo chema,
Na wasiwe na nakisi, hadi siku ya kiyama,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Wafanze wawe wasusi, kubuni yaliyo mema,
Kuwafaa kina nasi, kwa yako wewe huruma,
Wazikwepe na nuksi, ya adha nazo homa,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Ah, Yarabi ya Qudusi, ya Karima ya Rahima,
Iwe dahari nahisi, moto siku ya kiyama,
Niililie firdausi, ilmu nikiisoma,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Sunday, October 9, 2011

Mwananchi sasa hongera

Na twalikitatizika, kunako siku za nyuma,
Na wengine kuudhika, kurasa mlipotunyima,
Kwaisha kunung'unika, mmetuona adhama,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Gazeti linasifika, kot Afrika nzima,
Sanaa yahitajika, kwalo msirudi nyuma,
Ushairi kwa hakika, hufanza kitu kizima,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Gwiji wanayoandika, yanayo kubwa kalima,
Wananchi hujaongoka,wakazijua azma,
Na maisha huboreka, kujengeka nchi nzima,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Ushairi kuushika, ni kitu cha lazima,
Mbali nyie mtafika, wengine warudi nyuma,
Gazeti litauzika, mzijaze ndarahima,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Mtaamsha Afrika, Kiswahili kuwa chema,
Lugha ikajapanuka, kwenea dunia nzima,
Nakala zikauzika,hata Afrika nzima,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Waulize wenye rika, waandishi waadhama,
Mapinduzi kuja zuka, mchango walitwazima,
Kuwaenzi kina kaka,ushairi kuupema,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Kuasa wataasika, viranja na maamuma,
Nchi kutoterereka, tukawa taifa zima,
Hao wanaobweteka, kuwaamsha lazima,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Ili lugha kutumika, katika dunia nzima,
Mwananchi ni mshirika, kwa manufaa ya umma,
Nadhiri budi kuweka, lugha ngeni kututuma
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Kizungu tulikitaka, watoto wende kusoma,
Mambo yamebadilika, Uchina nako lazima,
India inatwalika, Aghakan keshasema,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!

Sisi tumefurahika, twawaombea uzima,
Mhariri mshirika, na wasanifu ulama,
Mashairi mtachoka, kwenu tutakavyoyatuma,
Mwananchi sasa hongera, kuuenzi ushairi!