Monday, October 10, 2011

Kwa shani wanaozuka

Ni asili na hulka, mwanadamu kumfika,
Kila anayeinuka, hutamani kusifika,
Na jinale kutajika, hata lisipohusika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Hawaachi kuzuzuka, kwa shani wanaozuka,
Iwe ni kwa kuandika, au nyimbo kuimbika,
Wote wanahadaika, wakidhani watukuka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Wale wachezao soka, asu sinema kuchezeka,
Haya pia huwafika, yakawa makubwa mashaka,
Huvianzisha vibweka, mijini wakatajika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Kila kizuri hutaka, na vyeo kujipachika,
Hata shule wasofika, uprofesa hutaka,
Wale wasioumbika, umalaika hutaka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Magari wakiyashika, hudharau zote rika,
Na ajali za kupika, haziachi kuwacheka,
Marehemu hugeuka, mkosaji kwa alofikwa,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Elimu yahitajika, vijana wetu kupika,
Waache kuja zuzuka, wawe wanaostahika,
Bilioni wakishika, wajue zinakohitajika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Msichana kusifika, si waume kukutaka,
Na mme kujatajika, si makoo yote kupoka,
Uungwana si dhihaka,na ukubwa ni mashaka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Maisha yana haraka, yanini kuhangaika,
Mbali hautofika, na dunia hukucheka,
Nayo japo waitaka, yenyewe haitakutaka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Zuzuka kwake Rabuka, nawe utatajirika,
Wala hutohangaika, na chochote kukitaka,
Utakuwa watosheka, japo umefilisika,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

Tukidhi mengi hakika, ila si ya kusifika,
Tunatambua Rabuka, ni wewe tu msifika,
Haya tunayoandika, ni kwako yanakotoka,
Kwa shani wanaozuka, hawaachi kuzuzuka!

No comments:

Post a Comment