Tuesday, October 18, 2011

Binadamu haridhiki

Haridhiki mwanadamu, maisha yake fataki,
Huyatamani matamu, japo kazi haitaki,
Hutaka kutakadamu, kuondoka haondoki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?


Hatosheki mwanadamu, kwa mamia na malaki,
Mtu asiyeisha hamu,kulimbikiza hachoki,
Ingawa linamgharimu,kwake halieleweki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Mwenyewe hujidhulumu, kwa zake tambo na ashiki,
Maisha huyahujumu, akidhani astahiki,
Cha halali na haramu, kwake havifahamiki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Mkweli humlaumu, akampenda mnafiki,
Udugu kwake haudumu, akapenda marafiki,
Wasafi huwatuhumu,akaamini mamluki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Mke aliye adimu, humfanzia mikiki,
Akamfata mndimu, mzinzi mwenye hilaki,
Huikataa salamu, matusi akaafiki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Wazazi hawarehemu, hutaka kutamalaki,
Kwayo anayojihimu, yote yanamdhihaki,
Kama analo jukumu, nafsi haishibiki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Muumba akimkarimu, vijisenti kwa malaki,
Hakai kujiheshimu, dharau atahakiki,
Shukrani huwa adimu, hata kwa wake Maliki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Magari atadhulumu, mengi akayamiliki,
Hata kuitoa dumu, ya kafara hudiriki,
Huidharau hukumu, akayajali lukuki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Majumba atadhulumu, kila pande amiliki,
Mengine akakasimu, kwa changu na mashabiki,
Akamhini karimu, himidi na tabaraki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

Nahofu yako hukumu, ewe Mujibu na Baki,
Nafsi nisidhulumu, nitosheke tu kwa hiki,
Kwa laili na kiamu, radhi yako na riziki,
Binadamu haridhiki, umpe nini atosheke?

No comments:

Post a Comment