Monday, October 10, 2011

Kulikoni ya ukwasi

Kulikoni wasiwasi, niepushe na dhuluma,
Siuhitaji ukwasi, nijalie wana wema,
Niepushe na kamasi, kuhesabu ndarahima,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Niepushe na yabisi, nipe moyo wa huruma,
Nifanze niwe msusi, wa kila jambo adhama,
Na nifanye mrahisi, kwa andiko na kalima,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Nusuru ngozi nyeusi, kwa wana walio wema,
Wape wakwangu sudusi, Alwaqiah kuzama,
Wawe watu wa kiasi, na wanyonge kutazama,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Wawe ni watu halisi, kuwajali mayatima,
Utu kwao udurusi, kwa zama mpaka zama,
Hadi siku abunusi, jichole kuwatazama,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Masikini wasiasi, kwao ni baba na mama,
Tulitoka huko nasi, mgongo kuwapa si vyema,
Wawashike kadamnasi, hata wasio heshima,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Wakinge na maasi, katika za kwetu zama,
Kwa tabia na libasi, wape kila kilo chema,
Na wasiwe na nakisi, hadi siku ya kiyama,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Wafanze wawe wasusi, kubuni yaliyo mema,
Kuwafaa kina nasi, kwa yako wewe huruma,
Wazikwepe na nuksi, ya adha nazo homa,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

Ah, Yarabi ya Qudusi, ya Karima ya Rahima,
Iwe dahari nahisi, moto siku ya kiyama,
Niililie firdausi, ilmu nikiisoma,
Nijalie wana wema, kulikoni ya ukwasi!

No comments:

Post a Comment